BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB), wakati wowote ndani ya mwezi huu inatarajia kutangaza sifa na vigezo vitakavyotumika kuwapangia mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 unaotarajia kuanza miezi michache ijayo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Dk Cosmas Mwaisobwa wakati akijibu maswali ya baadhi ya wateja waliotembelea banda la HESLB katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako HESLB inashiriki katika Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.
“Tunakamilisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka ujao wa masomo na tumepanga kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Julai tuwe tumeutangaza na tumefungua mtandao wetu ili waombaji wenye sifa waombe,” amesema Dk Mwaisobwa.
Amewataka waombaji wa mikopo watarajiwa wawe watulivu na kufuatilia kwa karibu vyombo vya habari na tovuti ya HESLB (www. heslb.go.tz) ambayo huwa na kiunganishi cha mfumo wa kuombea mkopo.
Awali, katika maonesho hayo, baadhi ya wananchi wanaotarajia kuomba mikopo ya elimu ya juu walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali yakiwemo tarehe ambayo Bodi itaanza kupokea maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Maswali mengine yaliyoulizwa ni pamoja na kama utaratibu wa udahili kupitia vyuoni moja kwa moja utaathiri upatikanaji wa mikopo. Pia baadhi ya wateja walitaka kupata elimu zaidi kuhusu taratibu za urejeshaji wa mikopo.
Akifafanua kuhusu maswali hayo, Dk Mwaisobwa amesema Sheria iliyoanzisha HESLB, pamoja na mambo mengine, inamtaka mnufaika kuanza kurejesha mkopo wake miezi 24 baada ya kuhitimu masomo.
source: habari leo
No comments:
Post a Comment